Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, mchezaji wa Akademi ya Alladini iliyopo
wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Ally Jacob Madanganya, ameuawa
kikatili kwa kuchomwa kisu na watu wasiojulikana na kufariki dunia papo
hapo wakati akiwa njiani kuelekea mazoezini.
Tukio
hilo lilitokea juzi jioni maeneo ya Majengo ambapo alikuwa akielekea
mazoezini kwenye Uwanja wa Halmashauri Kahama kujumuika na wenzake
katika mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Ligi Daraja la Nne Wilaya
ya Kahama.
Kocha
Mkuu wa Akademi Alladini, Imam Omary Mabrouk, alisema: “Mimi huwa nina
kawaida ya kufanya mazoezi mapema, hivyo wakati tukiwa uwanjani
tukiendelea na mazoezi, Ally ambaye ni mmoja wa wachezaji wangu,
alipatwa na mkasa huo kwa kuvamiwa na watu wasiojulikana
waliomshambulia.
“Tumesikitishwa
sana na tukio hilo la Ally ambaye alikuwa ni beki muhimu kikosini
kwetu, mara baada ya tukio hilo kuna mmoja wa wale waliomvamia
alikamatwa na wananchi na mpaka sasa yupo chini ya ulinzi wa jeshi la
polisi.
“Tunatarajia
kumpumzisha mwenzetu leo (jana), mambo mengine ya uchunguzi, sababu za
tukio hilo na usalama yanaendelea kufanywa na polisi.
“Ally
alikuwa na miaka 17, nilizungumza na baba yake alisema wanaye walikuwa
wakilalamika kufuatwafuatwa na watu wasiowajua lakini hakutilia maanani,
hivyo tukio hilo limemfanya kuhisi kulikuwa na uhusiano baina ya
alichoelezwa na wanaye na tukio hilo.”
SOURCE: CHAMPIONI