Siku moja kabla ya Yanga kuivaa Azam katika mechi
ya Ngao ya Jamii, uongozi wa Yanga umefanya tukio ambalo ni kama unataka
kurejesha hamasa ya ushindi ambapo umemwaga fedha za usajili ambazo walikuwa
bado wanadaiwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.
Yanga itakipiga na Azam, kesho Jumamosi kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo ni lazima timu moja ishinde ikiwa
ni ishara ya kufungua Ligi Kuu Bara 2015/16.
Awali, wachezaji hao kabla ya kulipwa fedha hizo,
walipanga kucheza chini ya kiwango kwenye mchezo huo baada ya kuona wachezaji
wenzao wa kigeni wamelipwa stahiki zao akiwemo beki wa kati raia wa Togo,
Vincent Bossou na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko ‘Ras’.
Baadhi ya wachezaji waliokuwa wanadai ni; Salum
Telela, Simon Msuva, Kelvin Yondani, Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius
Munishi ‘Dida’, Pato Ngonyani, Juma Abdul na Said Makapu.
Chanzo cha habari kutoka Yanga kimeeleza kuwa,
mabosi wa timu hiyo waliamua kukamilisha malipo hayo juzi Jumatano kwa kusaini
hundi ya malipo ili kuondoa mgawanyiko uliokuwa unaelekea kutokea.
“Uongozi umekamilisha malipo ya wachezaji wetu
13 waliokuwa wanadai fedha za usajili za msimu huu ambazo tulikuwa
hatujawakamilishia.
“Hiyo yote imefanyika kurejesha morali kuelekea
mechi yetu dhidi ya Azam, ninaamini hakutakuwa na visingizio na lawama kwa
wachezaji wetu na kama kufungwa tufungwe kimchezo na siyo kisingizio cha
kutowamalizia fedha zao za usajili,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas
Tiboroha kuzungumzia suala hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.