MIAKA mitatu iliyopita nilimuona kwa mara ya kwanza huyu dada anayeitwa Faiza Ally, hotelini De France, pale Sinza jijini Dar es Salaam. Aliyenikutanisha naye ni Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chadema.
Mbilinyi, mkongwe wa Hip Hop aliye miongoni mwa alama za Bongo Fleva, ambaye wengi tunamfahamu zaidi kama Sugu, ni mmoja kati ya mastaa niliopata kuwa nao karibu, hata baada ya kazi. Alinitambulisha kwake kama shemeji, kwa maana kuwa alikuwa mtu wake!
Baada ya hapo nimewahi kukutana naye mara kadhaa, mara moja kati ya hizo mjini Dodoma, wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba akiwa na Sugu. Sijapata kumuona akijihusisha na shughuli yoyote ya kisanii, kama uimbaji, uanamitindo au uigizaji.
Niwe mkweli, mara zote ambazo nilikutana naye, nilimwona kama mmoja kati ya wasichana ambao walistahili kuwa wameolewa ‘wife material’. Kwa jinsi nilivyomfahamu kidogo Sugu, niliamini kabisa yeye ndiye atakuwa chanzo cha kutengana kwao, maana mtu wa namna yake, kuishi na msichana mpole kama Faiza, kidogo ni tatizo.
Na sikushangaa niliposikia wametengana, ingawa tayari walikuwa wamejaaliwa mtoto Sasha. Sijawahi kuzungumza lolote na Sugu kuhusu kilichotokea, ingawa aliahidi kunipa mkanda kamili siku itakapofika. Ninasikitika hadi ninapoandika maandishi haya, bado hatujapata nafasi.
Faiza alianza kutumia akaunti yake katika mitandao ya kijamii kumlaumu mzazi mwenzake, kitu ambacho kwangu ni cha kawaida. Lakini nilianza kumtilia shaka siku aliyofanya sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, iliyofanyika Hoteli ya Sea Cliff, Dar es Salaam mwaka jana.
Shemeji yangu aliingia ukumbini akiwa amevaa Pampers, zile nepi wanazovalishwa watoto wachanga kuwakinga na mikojo. Ndiyo, ni mitindo ya akina dada wa kisasa kutaka watoke vipi ili kuwa tofauti, lakini staili hii, hapana.
Mei mwaka huu, kwa mara nyingine, Faiza aliniacha midomo wazi baada ya kuingia katika hafla ya Zari All White Party, iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, akiwa amevaa shati pekee, jeupe bila nguo nyingine yoyote.
Lakini kama kuna mtu alikuwa na shaka na tabia zake, atakuwa ameelewa kilichomo kichwani mwa Faiza baada ya wiki iliyopita kuingia ukumbini Mlimani City wakati wa utoaji wa Tuzo za Kili Music Award 2015, akiwa amevaa gauni la ajabu. Lilikuwa likionesha ‘live’ makalio yake!
Ni fasheni? Ni umjini? Ni usichana wa kisasa? Hapana, huu ni ujinga uliopitiliza. Mwanamke mwenye mtoto, tena aliyezaa na Mheshimiwa Mbunge, hawezi kujidhalilisha namna hiyo. Huenda hajui tu, lakini anamjengea mazingira magumu sana Sasha ukubwani.
Ni jambo la ajabu kwamba kwa taifa linalojali maadili yake kama Tanzania, Faiza aliachwa akatize mbele ya halaiki pale Mlimani City, huku baadhi ya watendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakimuangalia.
Faiza haoneshi fasheni, bali anawathibitishia watu kwamba Sugu alikuwa sahihi kumtema, bila kujali sababu yoyote anayoweza kuwa nayo.
Hivi, anawapa faraja gani marafiki walioumia baada ya kugombana na mzazi mwenzake?
Na kama nilivyosema pale mwanzo, anamjengea mazingira magumu sana mwanaye Sasha, ambaye haelewi lolote kwa sasa. Siyo suala la malezi, huu ni ujinga binafsi wa Faiza kwa sababu siamini kama kuna familia za Kibongo zinazoweza kuruhusu watoto kuwa na tabia kama hii, maana ni zaidi ya wale wavaa nusu utupu wa Bongo Movie!

AddThis

 
Top