Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa
amezungumza mambo mengi muhimu wakati alipokutana na waandishi wa habari kwa
mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kuinoa timu hiyo.
Pamoja na mambo mengi aliyezungumza Mkwasa, haya
mawili ni kati ya yale yaliyokuwa muhimu na huenda Watanzania tunapaswa kuyapa
nafasi.
Kwanza lilikuwa ni lile la kuwapa nafasi vijana wa kikosi
chake kwa kuwa ndiyo wanaanza kujipanga.
“Wavumilieni kwa kuwa sasa ndiyo wanajipanga upya
tena. Waungeni mkono na msitumie muda mwingi kuwazoemea au kuwapiga.
“Nafikiri hatuko katika hali ambayo tunaweza kusema
tumekaa vizuri, tunahitaji kujipanga. Tafadhari tupeni muda,” alisema Mkwasa.
Lakini la pili ni lile ambalo wakati anazungumza,
aliwagusa na Simba.
“Nitapita hadi kwenda mazoezi ya baadhi ya timu kwa
ajili ya kuangalia wachezaji. Lengo ni kupata wale wenye kiwango chenye msaada.
“Ninaweza kuzungumza na makocha wa timu mbalimbali
pia. Mfano naweza kuwatembelea mazoezini na kushauriana nao.
“Sasa si Simba mnione mazoezini kwenu, halafu mnipige mawe kwamba nimeijia nini. Mimi ni kocha wa timu ya taifa,” alisema Mkwasa.
Mkwasa bado ni kocha msaidizi wa Yanga na pia ni mmoja wa wachezaji magwiji wa Yanga.