Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm (kulia)

Michuano ya 40 ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati, (Cecafa Kagame Cup) inayoshirikisha timu 13 mwaka huu inaanza  kutimua vumbi leo jijini Dar es salaam.
Mashindano haya ambayo yanashirikisha timu 13 mwaka huu yamedumu kwa muda mrefu, ila kwa bahati mbaya yamekuwa na muonekana ule ule, hayana mvuto mbele ya mashabiki wa soka.
Mechi za ufunguzi leo uwanja wa Taifa ni APR ya Rwanda dhidi ya  Al Shandy ya Sudan saa 8 kamili mchana, KMKM ya Visiwani Zanzibar inaivaa Telecom ya Djibout  uwanja wa Karume saa 10 jioni, huku wenyeji Yanga wakiikaribisha Gor Mahia kutoka Kenya saa 10 jioni.

Kuelekea mechi ya Yanga na Gor Mahia, kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema: 

“Nimekuwa Afrika tangu mwaka 1996 hivyo nina uzoefu na soka la timu za hapa kwa muda mrefu, tumefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuikabili kila timu kwenye michuano hii. Kitu kikubwa ni kwamba, mimi huwa sidharau mpinzani wangu kwasababu kwenye soka lolote linaweza kutokea na hakuna mtu anayejua matokeo”, amesema Pluijm.
Kocha mkuu wa Gor Mahia Frank Nuttal akizungumza na waandishi wa habari
Kwa upande wake kocha mkuu wa Gor Mahia,  Mscotish  Frank Nuttal amesema yeye hana uzoefu mkubwa na soka la Afrika ukilinganisha na mpinzani wake (Van Pluijm) lakini amesisitiza kuwa vijana wake wako vizuri kuikabili Yanga leo uwanja wa Taifa.
“Yanga ni timu kubwa japo sijawahi kuiona ikicheza lakini naamini ni timu yenye ushindani na mechi ya kesho itakuwa ngumu lakini mwisho wa mchezo tutajua matokeo”, amesema kocha huyo.

Kwa faida yako msomaji,  michuano ya mwaka huu ina makundi matatu ambapo kundi  A lina timu za Yanga (Tanzania Bara), Gor Mahia (Kenya), Telecom (Djibout), KMKM (Zanzibar), Khartoum-N (Sudan).
Kundi B linajumuisha klabu ya APR (Rwanda), Al-Shandy (Sudan), LLB AFC (Burundi), Heegan  FC (Somalia).

Kundi C lina timu za Azam FC (Tanzania), Malakia (Sudan Kusini), Adama City (Ethiopia) na KCCA (Uganda).

AddThis

 
Top