Mbali na kufanya programu ya mazoezi ya gym, Idd tayari ameruhusiwa kuanza mazoezi madogo madogo ya kucheza na mpira na kukimbia mwanzoni mwa wiki hii huku Kimwaga akiendelea na mazoezi ya gym aliyoanza mwezi mmoja uliopita.
Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa amesema kuwa wachezaji hao wapo kwenye kipindi cha mwisho cha tiba yao cha kuwarejesha katika hali yao ya kawaida huku akidokeza Idd ataendelea na programu hiyo na anatarajiwa kurejea dimbani kuanzia Januari Mosi.
“Kimwaga kidogo kumetokea matatizo kidogo katika ukunjaji wa goti lake baada ya operesheni kwa hiyo sasa hivi bado anafanya mazoezi ya kukunja goti na pindi atakapokuwa ameweza kukunja goti vizuri naye ataruhusiwa kuanza kucheza mpira kidogo kidogo na kukimbia naye pia tutamtarajia itakapofika Januari Mosi atarudi tena kiwanjani kwenye ushindani,” alisema.
Idd anasumbuliwa na majeraha ya nyonga yake ya mguu wa kulia huku Kimwaga akisumbuliwa na goti la mguu wa kushoto kwa pamoja walifanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini na tokea waanze mazoezi ya gym wamekuwa chini ya uangalizi wa daktari wa Azam FC na wataalamu wa Kliniki ya London Health Centre, iliyopo eneo la Macho, Msasani jijini Dar es Salaam wanakofanya mazoezi ya gym.