Klabu za Simba na Yanga, zipo kwenye vita kubwa ya kumwania kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Mohamed Issa 'Banka' katika kipindi cha dirisha dogo la usajili ambalo linatarajiwa kufunguliwa Jumatano ijayo.
Kocha wa Yanga George Lwandamina, amevutiwa na kiwango cha mchezaji huyo kutoka Visiwani Zanzibar, amesema pamoja na kamati yake ya Usajili kuwa ihakikishe wanakamilisha zoezi la usajili wake mapema na hatimaye mzunguko wa pili avae jezi za njano na kijani lakini mahasimu wao Simba nao wameonekana kuhitaji huduma ya mchezaji huyo ambaye ndiyo anacheza ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza.
Yanga ndio wanaonekana kwenda resi na pengine ndio wanaelekewa kufanikiwa baada ya uongozi wa Mtibwa Sugar, kukiri kuwa wapo tayari kumuachia mchezaji huyo kwa timu yoyote ambayo itakuwa ya kwanza kukaa nao mezani na kumalizina.
"Tumesheanzisha mazungumzo na Mtibwa Sugar kuhusu usajili wa Banka, naamini hadi dirisha litakapofunguliwa atakuwa mali ya Yanga, kutokana na juhudi ambazo tunazifanya ili kumridhisha kocha wetu, ambaye ameonyesha kumuhitaji sana mchezaji huyo, amesema Katibu Mkuu wa Yanga Bonifave Mkwasa.
Kiungo huyo pamoja na ugeni aliokuwa nao kwenye ligi ya Tanzania Bara, lakini amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho kiasi hadi cha kujumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania bara, ambayo imekwenda nchini Benin, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wakimataifa uliopo kwenye kalenda ya FIFA.
Kama Yanga watafanikiwa kumpata mchezaji huyo itakuwa wamewapiga bao mahasimu wao Simba, ambao katika misimu miwili iliyopita asilimia kubwa ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza wamewachukua kutoka Mtibwa Sugar, akiwemo Shiza Kichuya, Mzamiru Yasini, Salum Mbonde Ally Shomari na kipa Said Mohamed.

AddThis

 
Top