Mshambuliaji
Papa Niang amepewa Jumatatu kama nafasi ya kuwadhihirishia Simba kwamba
ana uwezo na atakuwa msaada, hivyo chaguo lake, ashindwe arudi Senegal,
afanye vitu apande meli ya Simba.
Niang
raia wa Senegal ambaye amewasili nchini jana na kujiunga na Simba,
anasubiri siku hiyo ambayo Simba itacheza na MWadui FC kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam, kumshawishi kocha Dylan Kerr na benchi zima
la ufundi kwamba anaweza.
Lakini
Niang ataitumia nafasi hiyo pia kuwashawishi viongozi wa Simba kwamba
wanastahili kumwaga mamilioni ili kupata saini yake.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kila kitu kuhusiana na mechi hiyo kimekamilika.
“Ni
kweli mwalimu atamtumia Papa Niang ikiwa ni sehemu ya majaribio yake
mafupi na kupata uhakika kuwa ni mshambuliaji wa kiwango tunachotaka.
“Pia
tunaamini ni nafasi ya mashabiki wa Simba kumuona mchezaji huyo na
kikosi chao kwa ujumla na wanaweza pia wakawa na mchango wao,” alisema
Kaburu.
Kuhusiana
na mechi kuchezwa Jumatatu, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Simba, Haji
Manara amesema inawezekana ikawa tofauti lakini ndiyo mabadiliko ya
kisoka duniani.
“Unajua
England sasa wana mechi zinazochezwa Jumatatu, hizo ni mechi za Ligi
Kuu England. Hapa pia tutaenda tunabadilika taratibu na itawezekana.
“Tunaamini
kunaweza kuwa na usumbufu kidogo, lakini tutaenda tunazoea.
Ninachowashawishi mashabiki wa Simba, wapenda mpira wote wafike
uwanjani.
“Pia
kutakuwa na nafasi ya kumuona mshambuliaji Papa Niang akiichezea Simba,
pia kupata uhakika kutokana ana uwezo wake,” alisema Manara.