TAIFA
Stars imepata bosi mpya, safari hii kwa mara nyingine ni mzawa, Charles
Boniface Mkwasa ambaye ni kocha msaidizi wa Yanga.
Mkwasa
atakuwa anasaidiwa na mzawa mwingine, Hemed Suleiman, maarufu kama Morocco. Sasa
ni timu ya Watanzania inayoongozwa na Watanzania.
Waandishi
kazi yetu kuchimba, nilizipata taarifa hizo mapema sana, kwangu ikawa ni
kusubiri kama kweli TFF watakuwa na uthubutu huo wa kumrudisha mzawa katika
nafasi hiyo kubwa kabisa.
Mara
baada ya kutangazwa, utani kwenye mitandao mbalimbali ukaenea. Eti, Rais wa
nchi-Yanga, Rais wa TFF-Yanga, Nahodha wa Taifa Stars-Yanga, bingwa wa
nchi-Yanga, sasa na Kocha Taifa Stars-Yanga!
Soka
lina raha yake, utani ni kitu cha kawaida, lakini mimi nikajua Mkwasa
ninayefahamu utendaji wako, kamwe hauwezi kuwa na utani kwa kuwa unaelewa nini
maana ya timu ya taifa.
Kamwe
siwezi kupoteza muda kukufundisha kuhusiana na uzalendo, umeichezea Yanga
katika michuano ya kimataifa ukiliwakilisha taifa, lakini umeichezea Taifa
Stars, hivyo kwangu niseme nikaona ni uchaguzi mwafaka katika kipindi hiki.
Lakini
nikaona ndiyo wakati mwingine tena wa kujifunza tukiwa na kocha mzawa kwa kuwa
sasa imekuwa kitambo, makocha wageni wamekuwa wakituongoza huku “tukipigwa tu”.
Mara
ya mwisho, Stars iliongozwa na mzalendo, Mshindo Msolla. Baada ya hapo, ikawa
ni makocha wa kigeni kubadilishana hatua kwa hatua wakianzia na Marcio Maximo.
Maximo
alitua nchini Juni, 2006 hadi sasa 2015 ni miaka tisa, hatujawahi kuwa na kocha
mzawa wa kikosi cha Taifa Stars. Mkwasa unarejea tena kuwa mzawa, tena
ukisaidiwa na mzawa mwingine.
Stars
imepita kwa wageni kwa miaka tisa, Maximo kutoka Brazil, Jan Poulsen na baadaye
Kim Poulsen kutoka Denmark na baadaye Mart Nooij (Uholanzi).
Mafanikio
makubwa kama mabadiliko ambayo iliyapata Stars, ilikuwa ni kushiriki michuano
ya Chan kule Ivory Coast wakati wa Maximo. Baada ya hapo, kumekuwa na
mabadiliko madogomadogo sana labda kupatikana kwa wachezaji makinda na
vinginevyo.
Ukiachana
na hivyo, hakuna tofauti kubwa sana kwa maana ya mafanikio, labda mabadiliko
kwenye sura ya timu kwa maana ya udhamini mnono ambao umekuwa ukifanya timu
iweke kambi katika hoteli kubwa na bora, wachezaji wapate posho angalau nzuri,
usafiri safi na viwanja vizuri vya mazoezi, hali kadhalika vifaa wanavyotumia.
Tena
tumeambiwa utakuwa ukilipwa donge nono la mshahara wa dola 12,000 (zaidi ya Sh
milioni 27) kwa mwezi alizokuwa akichota ‘babu’ Nooij. Unakuwa kocha wa kwanza
mzawa kulipwa fedha nyingi kama hizo ukiwa na Taifa Stars.
Kitita
hicho kwa mwezi si kwako wewe tu kocha, naamini hajawahi kulipwa yeyote hasa
kwa wazawa katika mchezo wa soka au mingine. Maana yake kwa sasa wewe ndiye
mwanamichezo ghali kuliko wengine Tanzania. Hongera kaka, ingawa nasikitika
sikudai, maana huu ungekuwa muda mwafaka.
Dhumuni
la barua hii ni kukukumbusha mambo mawili matatu, kwamba Watanzania wa sasa si
wale wa zamani. Kweli ni wazalendo na nikuhakikishie kwamba wanaipenda sana
timu yao. Hivyo lazima ukubali kuwa kweli muda unatakiwa lakini si muda mwingi
wa mwendo wa kobe.
Kamwe
Watanzania hawawezi kuiona Stars ikiboronga kwa miezi 12 wakakaa kimya kwa kuwa
wewe ni mzawa.
Nilitamani
nikunong’oneze hata nisiandike hapa. Kwamba nafasi umeipata, huenda huu ndiyo
wakati mwafaka wa kuwazika kabisa makocha wa kigeni.
Mwambie
Morocco kuwa mfanye kweli ili TFF na wadau wengine wawasahau kabisa makocha wa
kigeni. Rungu liko mikononi mwenu, kazi kwenu mchague mpige upande upi kumaliza
‘mchezo’.
Nimesafiri
nawe zaidi ya mara tatu ukiwa na Twiga Stars iliyokuwa ina maandalizi lakini
haipati kila kitu, lakini ilifanya vizuri, kumbuka tukiwa Ethiopia, tulipata
ushindi wa kishindo na timu ikacheza Kombe la Mataifa Afrika.
Najua
unaweza, lakini changamoto zitakuwa nyingi. Wabongo wenzangu nimewashauri
tukuunge mkono, lakini lazima ukubali kwamba kazi uliyonayo ni kubwa na kamwe
hauwezi kuwa na visingizio.
Hauwezi
kusema hatuna wachezaji, najua hauwezi kusema hatuna uwanja mzuri wala vifaa au
sehemu nzuri ya kuweka kambi. Kama ni posho, waambie wawahishe wasiue morali. Halafu
kamua, wamalize wageni na uzike miaka tisa ya mapito yao.
Ushauri
mwingine mdogo, usikubali kuyumbishwa na Uyanga na Usimba. Angalia kilicho
sahihi, fanya kwa faida ya taifa.
Kumbuka,
ukishindwa wewe safari hii, basi huenda ukawa ndiyo mwisho wa wazawa kuinoa
Taifa Stars kwa miaka mingine tisa ijayo au zaidi. Rungu ulilopewa ni kuipa
heshima Stars na taifa letu, lakini kuwapa heshima makocha wazawa.
Mimi
hata sifichi, ninakuunga mkono wewe na wote katika kikosi chako, lakini
mkishindwa, mkazidi kuboronga nje ya uvumilivu, nageuza gari, kazi inaanza.
Nawatakia
kila la kheri, ila nakukumbusha wewe na wenzako, maumivu ya moyo yamekuwa
makubwa mno, ya muda mrefu mno, tupunguzieni.