Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limekubali kuongeza idadi ya wachezaji wa kulipwa kutoka watano hadi saba kwa msimu ujao wa 2015-16.

Timu zimepewa nafasi ya kuwatumia wote saba kwa wakati mmoja kama zitaona ziko tayari kufanya hivyo. Tayari suala hilo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka.
Kila mmoja ana maoni yake ambayo ni haki yake kufanya hivyo. Kwangu binafsi nilitaka kujifunza zaidi, kwamba kwa wachezaji hao, kiwango chetu kitapanda au kudorora?
Wakati mwingine ni vizuri kujifunza kwa vitendo, kwani pamoja na uwezo wa wachezaji watano, bado sikuona mabadiliko makubwa ya ukuaji wa kiwango. Je, hawa saba watatusaidia kukipandisha au tutaboronga zaidi?
Ninaamini kama tutaona ni tatizo, kikubwa TFF inatakiwa kuwa na utayari wa kubadili kanuni na kupunguza. Kama itakuwa na faida, basi iachwe iendelee, kikubwa ukweli upewe nafasi katika hilo na kusiwe na maslahi binafsi.
Hakuna anayeweza kupinga kwamba Yanga, Simba na Azam FC ambao ndiyo wakubwa wamekuwa chagizo la uongezwaji wa wachezaji hao wa kigeni. Hata ukisema ni kamati ya utendaji ya TFF, lazima tukubali ina watu wake humo ndani ambao walisaidia kwa ushawishi kufanikisha hilo.
Lakini sasa TFF pamoja na kupitisha hilo, imeibuka na jambo jipya kabisa. Kwamba kila mchezaji mmoja wa kigeni, anapaswa kulipiwa dola 2,000 (zaidi ya Sh milioni 4) kwa msimu mmoja! Kwangu ni kichekesho.
Katika hili huenda ikawa ni ushamba wangu, lakini nimeshangazwa na ukimya wa Yanga, Simba na Azam FC, wamekaa kimya huenda kwa kuwa wako kwenye sherehe ya kuruhusiwa kutumia wachezaji saba.
Ninaamini baada ya miezi mitatu minne mara baada ya kuanza msimu, Yanga, Simba, Azam FC wataanza kulalama kuhusiana na kodi hiyo ya TFF ambayo tumeelezwa inakwenda kusaidia soka la vijana.
TFF haikupaswa kuzitoza Yanga, Simba, Azam FC na klabu nyingine fedha kwa ajili ya kuendeleza vijana kwa kuwa zinatoa tozo la mfuko wa maendeleo ya michezo kila zinapocheza mechi.
Badala ingekaa nazo na kuzipa mkakati tena kwa ulazima kwamba zinatakiwa kuwa na timu za vijana na TFF ianzishe ligi maalum ili kuzibana katika hilo ili kuwa na Tanzania inayokuza warithi wa waliopo sasa.
Pia TFF haikupaswa kuzilipisha klabu kwa kuwa wachezaji hao wanalipiwa kodi za serikali hasa kibali cha kufanya kazi nchini. Bado TFF imesahau kuwa uwezo wa wachezaji wa kigeni unaisaidia yenyewe na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kupata fedha zaidi kwa kuwa watu watakwenda uwanjani kwa wingi kutaka kuwaona.
Lakini wanaowagharamia kila kitu kuanzia mishahara, makazi, posho na kila kitu ni klabu. Hivyo kuna kila sababu ya kuzisaidia klabu kupunguza gharama zisizokuwa na sababu ya msingi.
Bado kuweka ada kubwa kama hivyo kwa mchezaji mmoja wa kigeni ni kuzitisha au kuzilazimisha timu nyingine ukiachana na vigogo hao, kushindwa kuwa na wachezaji wa kigeni.
Hatuwezi kusaidia kukua kwa soka ya Tanzania kwa uoga na kusukuma wenye changamoto wasije. Acha waje tuone kama wanatusaidia, wachezaji wa Tanzania nao wapambane kutafuta njia ya kutoka si kung’ang’ania nyumbani wakionyesha wana woga wa ushindani.
Nje wanaogopa kwenda, hawataki kupambana pia ni waoga. Nyumbani pia hawataki kupata ushindani, sasa nao ni watu wa aina gani hawa?

Inawezekana madhara ya hili yasionekane sasa, lakini taratibu uzito wa mzigo huu utaanza kuonekana kadiri siku zinavyosonga mbele. Hivyo nashauri, vema hilo likaangaliwa mapema na vizuri TFF kama mzazi kujali suala la kuzipunguzia mzigo wa kifedha klabu maana ndizo zinazoifanya TFF na TPLB ziwepo. Kama Simba, Yanga na klabu nyingine, hakuna vyombo hivyo.

AddThis

 
Top