Kikosi
cha England cha U21 kimeambulia kipigo cha nguvu kutoka kwa Italy
kwenye mchezo wa kundi B kwenye michuano ya Mataifa ya Ulaya kwa vijana
wenye umri wa miaka chini ya 21 (Ueropean Under 21 Championship)
inayoendelea huko Jamhuri ya Czech.
Andrea
Belloti alianza kuiandikia Italia goli la kwanza dakika ya 25
akimalizia kazi safi iliyofanywa na Domenico Berardi, dakika mbili
baadae (dakika ya 27) Marco Benassi aliifungia Italia goli la pili na
kuufanya mchezo kwenda mapumziko huku Italia ikiongoza kwa goli 2-0n
mbele ya Uingereza.
Dakika
ya 72 kipindi cha pili mambo yalizidi kuwa magumu kwa Uingereza kwani
Marco Benassi alipachika bao la tatu kwa upande wa Italia na kuwaduwaza
vijana wa Uingereza waliokuwa wamekomaa wakitaka kupata magoli ya
kusawazisha. Uingereza walipata goli lao la kufutia machozi dakika ya 90
kupitia kwa Nathan Redmond na kuufanya mchezo huo kumalizika Italia
ikiwa mbele kwa goli 3-1 dhidi ya Uingereza.
Kichapo
hicho kimeifanya Uingereza kutupwa nje ya michuano hiyo baada ya
kumaliza mkiani mwa kundi B ikiwa na pointi tatu nyuma ya Italia yenye
pointi nne, wakati Sweeden wao wako nafasi ya pili wakiwa na pointi nne
huku Ureno ikiwa ni kinara wa kundi hilo ikiwa na pointi tano.