Na Makongoro Oging’

MAAJABU ya Mungu! Ukisema wewe unaumwa sana, inawezekana hujawaona wagonjwa wengine! Faiza Masaka Paga (23)(pichani), mkazi wa Chanika –Msumbiji, Ilala jijini Dar amekumbwa na gonjwa la ajabu ambalo mpaka sasa madaktari hawajajua ni nini kwani sehemu ya kiuno na kalio upande wa kushoto imevimba na kumfanya aonekane ana kama nundu kubwa ya kutisha!
Faiza Masaka mkazi wa Chanika akionyesha jinsi uvimbe huo ulivyo kwenye mwili wake.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwa mfadhili anayeishi naye huko Chanika, Faiza alisema tatizo hilo lilimuanza mara tu baada ya kupata ujauzito, Mei mwaka jana.
 
.......akionyesha jinsi uvimbe huo ulivyomkubwa na unavyomsumbua.
MSIKIE MWENYEWE
“Ilikuwa mwaka jana, nikiwa mjamzito wa huyu mwanangu (aliyempakata pichani mbele). Sehemu hii ilianza kwa kuvimba kitu kama kipele, baadaye kikawa kinakua kwa kasi mpaka nikaogopa sana.
“Labda nianze kwa kusema hivi, kabla ya kuupata ugonjwa huu wa kushangaza, nilipitia mambo magumu na mazito, kumbe ilikuwa ni salamu kwa ajili ya tatizo hili.
“Nikiwa darasa la pili, Shule ya Msingi Mnazi Mmoja (Dar) baba aliugua, akawa haendi kazini. Maisha yakawa magumu. Ilibidi mama aanze biashara ya kuuza mahindi ya kuchemsha mitaani. Kuna wakati yakawa hayauziki na akirudi nayo ndiyo tuliyageuza chakula cha usiku. Nilipofika darasa la tatu, baba alizidiwa, akafariki dunia.
 
......akionyesha kwa upande wa nyuma jinsi uvimbe huo unavyoonekana kwenye mwili wake.
WAFUKUZWA KWENYE NYUMBA
“Nyumba tuliyopanga ikaisha kodi, mwenye nyumba akabaini kwamba mama hana huwezo wa kulipia tena, akatutimua. Tukawa hatuna pa kwenda. Ilibidi tuondoke Dar kwenda Tanga kwa bibi na babu wazaa mama. Walitukaribisha ingawa kulikuwa na mzigo mkubwa wa maisha.
 BABU AFARIKI DUNIA
“Kabla hatujakaa sawasawa, babu aliugua ghafla, akafariki dunia. Tukawa tunaishi kwa shida na bibi, hata kusoma kwangu kukawa kwa shida.”

......akiwa anamnyonyesha mtoto wake ambapo alipata uvimbe huo mara baada tu yakushika mimba yake.
MAMA, BIBI WAFARIKI DUNIA
Bado nikiwa katika mawazo ya maisha yangu ya baadaye hasa kuhusu elimu, mama naye aliugua akafariki dunia. Nikabaki na bibi tu.”
“Tukawa tunaishi kwa shida sana. Nilijitahidi kwenda shule ingawa wakati fulani nilikuwa nikishinda njaa. Lakini nilijua elimu ndiyo mkombozi wangu wa pekee baadaye. Mwaka 2012 bibi alipatwa na presha, akafariki dunia. Nikabaki peke yangu pale nyumbani.”
“Nilijua ndiyo mwisho wa maisha yangu kwa vile niliamini sitasoma tena. Hapo sikuwa na wazo kwamba kuna kubwa zaidi linaningoja mbele, yaani hili la huu ugonjwa wa ajabu.”
 MWANAUME AJITOKEZA
“Mwaka 2014, nikiwa mtu wa kutangatanga kulekule Tanga, alitokea kijana mmoja, akanirubuni nikaishi naye kwake ili anioe. Nilimkubalia, sikuwa na jinsi. Nikiwa ndani ya uhusiano, nikapata mimba. Lakini mimba hiyo ikaenda sambamba na uvimbe. Ukawa unakua kwa kasi.
“Kuona hivyo, yule kijana aliondoka nyumbani. Nikawa sina mtu wa kunipeleka hospitali, sina pesa ya matibabu wala chakula.”
 MWANAUME HAPOKEI SIMU
“Siku moja niliamua kumpigia simu, akapokea lakini akaniambia hawezi kurudi nyumbani, nitafute pa kwenda. Nilikonda sana. Nikaanza kuomba nauli kwa watu, nilipopata nikaja Dar kwa rafiki wa mama anayeishi Chanika.
“Yule mama aliponiona na uvimbe alitokwa machozi. Pia  kutokana na afya yangu kwani nilikuwa na mimba kubwa huku uvimbe nao ukikua sana. Niliishi kama mnyama asiyepata matibabu.
“Sasa uvimbe ulikua kiasi kwamba, nilishindwa kuvaa suruali, magauni nayo yakawa yanatoa kinundu. Watu walianza kunishangaa. Usiku nashindwa kulala kwa maumivu makali.
 APELEKWA MUHIMBILI
“Rafiki wa mama anajishughulisha na biashara ya kuuza karanga kwa kufunga za miamia. Mume wake hana kazi, lakini alinichukua na kunipeleka Muhimbili. Walinichunguza na kuniambia inabidi nijifungue kwanza ndipo mambo mengine yaendelee.
“Februari 6, mwaka huu nikajifungua kwa njia ya upasuaji. Hali yangu ilizidi kuwa mbaya kiafya. Madaktari wakaniambia nisimnyonyeshe mtoto. Ikawa gharama nyingine, kununua maziwa, pesa hamna kwani kuna wakati karanga hazinunuliwi.
“Mpaka sasa hivi nasubiri kama nitapatiwa matibabu na madaktari. Ingawa hata nikibahatika kupata matibabu sijui nitaishi vipi. Naumwa sana Watanzania wenzangu, naomba mnisaidie. Maisha yangu nayakabidhi mikononi mwenu,” alifunga kusema Faiza huku machozi yakimbubujika.
 BABA MLEZI ANENA
Baba mlezi wa Faiza, Mohamed Mrisho ambaye mke wake alimpokea Faiza, kwa upande wake alisema kwamba siku binti huyo alipofika kwake akitokea Tanga yeye hakuwepo nyumbani. Aliporudi alikuta ugeni huo huku binti akiwa amechoka na mwenye maumivu makali.
“Hamna jinsi, inabidi nikae naye ingawa na sisi hapa uwezo wetu kimaisha si mzuri. Mgonjwa huyu anahitaji mambo mengi ukizingatia ana mtoto mdogo ambaye anahitaji matumizi, pia mama yake anahitaji fedha ya matibabu. Nawaomba wasamaria wema wamsaidie kwa hali na mali,” alisema baba mlezi huyo.
 KUTOA NI MOYO
Kwa yeyote mwenye huruma na moyo wa kumsaidia Faiza, anaweza kutuma chochote kwa kupitia njia ya simu kwa namba; 0787 853153, 0654 187240 au 0717 260769.

AddThis

 
Top