MUSONYE |
Na Saleh Ally
MICHUANO ya Klabu Bingwa
Afrika sasa ina miaka 42 tangu ianze. Rasmi ilianzishwa mwaka 1967, Abaluhya ya
Kenya ikashinda katika fainali dhidi ya Sunderland (Simba) kwa mabao 5-0 na
kubeba kombe.
Baada ya hapo, michuano
hiyo haikufanyika hadi mwaka 1974. Fainali ikawa pia Simba dhidi ya Abaluhya na
safari hii Msimbazi wakaibuka na ushindi na wakawa mabingwa wa kwanza wa kombe
hilo jipya.
Hadi sasa Simba ndiyo
mabingwa wa kihistoria ambao wamelibeba mara nyingi zaidi baada ya kulitwaa
mara sita lakini Kenya ndiyo nchi iliyolichukua mara nyingi zaidi kupitia klabu
mbalimbali.
Kenya imelibeba mara 15
kupitia klabu zake mbalimbali, inafuatia na Tanzania mara 11. Uganda
wamelichukua mara 5, Rwanda mara 4 na Sudan mara tatu tu.
Michuano hiyo ndiyo
mikongwe zaidi unapozungumzia ile ya ukanda, mfano wa Cosafa na mingineyo kwa
kuwa ilianzishwa kitambo zaidi.
Lakini ndiyo michuano ya
kanda au mikubwa inayoendeshwa kwa kusuasua, ujanja mwingi, haina mvuto,
ubunifu wala mabadiliko katika mambo kadhaa muhimu.
Ndiyo michuano ambayo
inakwenda kwa staili ya uongozi uleule miaka nenda rudi. Hakuna ubunifu kwa
maana ya kuwashawishi mashabiki kwamba ni michuano bora.
Hakuna ushawishi kwa
wadhamini kwamba michuano hiyo ni bora na wanaweza kujitangaza na kufanya
vizuri. Kawaida inaonekana ni kama mali ya Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya
Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye.
Musonye raia wa Kenya ndiye
kila kitu katika michuano hiyo. Yeye ndiye Katibu Mkuu wa Cefaca asiyeisha,
anaendelea kubaki hapo alipo. Anaendelea kufanya kazi kwa mfumo uleule wa miaka
ilee.
Ingawa rais na viongozi
wengine wamekuwa wakichaguliwa, lakini Musonye amekuwa ndiye mtu anayeongoza
zoezi hilo kwa kuwa ofisi za Cecafa sasa ni kama mali yake.
Zawadi za michuano hiyo
ambayo sasa maarufu kama Kagame zinatolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Rais
huyo anastahili pongezi kwa kumwaga dola 60,000 (Sh milioni 120) kila msimu wa
michuano hiyo.
Mshindi hupata dola 30,000,
mshindi wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000. Zaidi ya hapo ni hisani ya
wadhamini wengine kama wanajitokeza, basi zinaongezeka kama ilivyokuwa
ilipofanyika Sudan.
Michuano inayokutanisha
zaidi ya nchi tano, vipi iwe shida kupata wadhamini hata wanaoweza kuongeza
nguvu ya zawadi ili kuzihamasisha zaidi timu ya wachezaji.
Mfano Yanga ambayo
inajiandaa kucheza kimataifa, inapewa nafasi ya kutumia wachezaji 20 tu! Si sahihi
kwa kuwa timu zingependa kutumia wachezaji zaidi.
Udhamini unaibana Cecafa
ambayo inaonekana haiaminiki kwa wengi, ndiyo maana wanashindwa kujitokeza
kudhamini na kutoa fedha zao.
Angalia namna ambavyo
Cecafa imekuwa ikihaha kupata wenyeji wa michuano hiyo. Sasa kimbilio limekuwa
ni nchi za Tanzania na Rwanda. Uganda, Kenya, Burundi wamekuwa wakiikimbia.
Nikukumbushe kila
inapofanyika, imekuwa ikiacha deni kubwa kwenye hoteli na kwingineko. Hii ni sehemu ya kuonyesha maandalizi
yake ni ya kubabia.
Kama zawadi hazikui, kama
ubora wa michuano hauboreshwi na kwa nini Musonye ni yuleyule, kweli katika
ukanda wote huu hakuna mtu mwenye mawazo mapya anayeweza kusaidia kuleta
changamoto na mabadiliko mapya katika michuano hiyo inayoendelea kuthibitisha
kuwa kweli ni mikongwe lakini isiyokuwa kiubora.
Ukiambiwa michuano hiyo
imefika, hakika cha kwanza unajua umekaribia kumuona Musonye. Michuano
inaonekana kufanana naye, inatembea kama yeye, inaonekana kama yeye na huenda
itaendelea kubaki hivyohivyo kwa ajili yake yeye.
Sipendi wanaogeuza vitu vya
watu kama mali yao. Angalau maendeleo au mafanikio ya michuano hiyo yangekuwa
makubwa hadi katika michuano mikubwa kama ya Afcon au Chan. Lakini hakuna
lolote, na sasa tunasubiri Musonye aje tena Tanzania kwa kuwa michuano hiyo
inaanza Juni 11 hadi Agosti 2.