Wakati uongozi wa Simba ukipanga kumfikisha kiungo wao, Ramadhani Singano ‘Messi’ katika kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), habari za chini ya kapeti zinaeleza kuna kitu kinaendelea kati ya mchezaji huyo na Azam FC.

Simba na Messi wapo katika mvutano mkubwa juu ya mkataba kutokana na pande mbili kupingana juu ya muda wa mkataba uliosainiwa, Simba ikidai ni miaka mitatu wakati mchezaji akidai ni miaka miwili.
Wakati hayo yakiendelea, mwishoni mwa wiki iliyopita, Singano alionekana kwenye ofisi za Azam FC zilipo Barabara ya Mandela licha ya katibu wa timu hiyo, Iddrisa Nassor kukanusha kuonekana kwa mchezaji huyo ofisini hapo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya timu hiyo zinasema tayari Singano ameshamalizana na Azam ambapo kinachosubiriwa ni kumaliza sakata lake la mkataba wa Simba ili atangazwe rasmi kama mchezaji mpya wa Azam FC.
“Imekuwa ni suala la siri lakini ukweli ni kwamba tayari Messi ameshamalizana na uongozi wa Azam FC ila kitu kinachokwamisha asitangazwe ni mgogoro wake wa kimkataba na Simba,” kilisema chanzo hicho.
Azam FC hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na ndivyo ilivyokuwa kwa Singano ambaye alisema suala hilo ameliweka pembeni kwa sasa.

SOURCE: CHAMPIONI

AddThis

 
Top