Kiungo wa Yanga, Mbrazili, Andrey Coutinho, jana Alhamisi alianza
mazoezi kwa mkwara mzito kwa kufanya mambo kadhaa yaliyoonyesha kweli
amejipanga na safari hii anataka kufanya kweli.
Kwanza Coutinho ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kuwasili uwanjani
huku akimfunga bao la kiwango cha dunia kipa, Ally Mustapha ‘Barthez’.
Coutinho, sambamba na mshambuliaji wa timu hiyo, Kpah Sherman, raia
wa Liberia, wamekuwa wachezaji wa kwanza wa kimataifa kuripoti kwenye mazoezi
ya timu hiyo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar chini ya kocha Hans van
Der Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa ‘Master’.
Coutinho aliingia uwanjani akiongozana na Sherman, ambapo
waliwasalimia wenzao wa benchi la ufundi, wakarejea kwenye gari kuchukua viatu
na kuanza mazoezi huku wachezaji wenzao wakiendelea kupiga soga, kitendo
kilichomkera Pluijm mpaka walipoitwa na Mkwasa kwa ajili ya kuanza mazoezi.
Katika mazoezi hayo, wawili hao walipewa programu maalum ya mazoezi
ambapo walianza kwa kutembea na baadaye kukimbia kabla ya kujiunga na wenzao
kwa mazoezi ya pamoja.
Mbali na hapo, Coutinho alimtesa Barthez kwa kufunga bao zuri baada
ya kutishia kama anapiga shuti kisha ‘akauchop’ mpira ambao ulitinga wavuni huku
kipa huyo akiwa hoi akishindwa kuamini kilichofanywa na Mbrazili huyo.
Mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo wakawa wanampigia makofi na
kumshangilia mara kadhaa kutokana na kuonyesha kujituma, lakini upande wa
Pluijm, akimzungumzia mchezaji huyo, alisema:
“Nimefurahishwa na kiwango cha Coutinho, anaonekana anajituma lakini
kuna baadhi ya vitu lazima avifanyie kazi ikiwemo kukaba akiwa uwanjani. Hilo
ni tatizo ambalo amekuwa nalo siku nyingi, anasaidia mashambulizi lakini hawezi
kukaba.”