SIKU kadhaa baada ya Shirikisho la Soka Tanzania
kuwakutanisha Ramadhan Singano ‘Messi’
na Simba katika kikao cha pamoja kujadili utata wa mkataba na pande zote
mbili kufikia makubaliano ya kuifuta mikataba yote na kuanza mazungumza mapya,
Mwanasheria Alex Mgongolwa ametumia dakika chache kueleza sakata hilo.
Kumbuka Singano anasema alisaini mkataba wa miaka miwili unaoisha
Julai 2015 wakati Simba wanadai nyota wao huyo alisaini miaka mitatu na mkataba
wake utaisha Julai 2016.
Kutokana na utata huo, TFF iliamua kuwakutanisha na kufanya
mazungumzo ya pamoja na kufuta mikabata yote, lakini ilishindwa kubainisha
mkataba upi ni halali na nani ameghushi.
Hapo ndipo hoja ya Msingi imesimama na watu wengi wanataka
kujua nani alihusika kughushi mkataba huo?
Katika kuendelea kupata ufafanuzi, Kituo cha Azam TV
kilifika ofsini kwa Mwanasheria Alex Mgongolwa ambaye amewahi kuwa mwenyekiti
wa kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji TFF ikitaka kujua kisheria suala hili
liko vipi .
Mgongolwa ametoa maelezo haya ya kisheria, tumia muda wako
kuyasoma;
“Yale yalikuwa ni maoni na ushauri kutoka sekretarieti ya
TFF, ukiangalia muundo wa katiba ya TFF imeainisha kwamba vitakuwepo vyombo au
kamati zitazokuwa na majukumu ya kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali yanayojitokeza katika kazi za
Shirikisho.
Ipo kamati ya ufundi ambayo hushughulikia masuala yote ya
ufundi, ipo kamati ya mashindano, ipo Bodi ya ligi, ipo kamati ya Sheria.
Suala la Ramadhan Singano 'Messi' ni suala ambalo lina
muonjo wa moja kwa moja wa kisheria. TFF ina kamati ya sheria ambayo wajibu
wake mkubwa ni kupitisha usajili na kuangalia masuala yote ya kisheria ikiwemo
katiba, kanuni na taratibu mbalimbali za TFF.
Kwa namna ambavyo maoni ya TFF yametoka, yanaweza kutumika kama ushahidi endapo upande
mmoja haujaridhika na ushauri ule waliopewa na kupeleka kamati inayohusika
ambayo ni kamati ya Sheria.
Ukiangalia ule ushauri au maoni, kwanza TFF inakiri kwamba
kwa wakati huu, Messi hana mkataba na Simba, kama angekuwa na mkataba, TFF
ingesema bayana kwamba Shauri hili limeletwa kabla ya wakati kwasababu wewe
mchezaji una mkataba na klabu yako.
Kipindi ambacho una mkataba na klabu
yako kinachohitajika kufanyika ni utekelezaji wa yale mliyokubaliana, lakini
mkataba huo unapokwisha ndipo kuna haja ya kuwa na makubaliano ya mkataba mpya.
Zipo kanuni mbalimbali zinazotawala wakati wa uingiaji wa
mkataba, kanuni kubwa ni ridhaa ya pande zote mbili, hata wakishauriwa kama
walivyoshauriwa, sheria inazuia watu kulazimishwa kuingia kwenye makubaliano.
Kwahiyo bado kanuni ile ya ridhaa itatumika, ikitokea kwamba
pande hizi mbili hazijakubaliana, basi hakuna kinachofanyika kulazimisha upande
mmoja uje katika makubaliano.
Kwa mujibu wa Sheria za CAF za mashindano, hata kule
kughushi ambako kumefanyika kwa bahati mbaya, yaani bila kujua, bila kuwa na
dhamira kuna adhabu yake. Unakumbuka
suala la Nurdin Bakari, ilidhihirika na CAF kwamba, kweli Tanzania tulitoa
taarifa za mchezaji ambazo si sahihi bila kudhamiria, adhabu iliyofuata pale ni
kutolewa katika mashindano.
Unajua dhana ya kughushi inajitokeza pale ambapo mmoja
anataka kupata faida kwa jambo ambalo katika hali ya kawaida lisingeweza kumpa
faida ile anayoitaka, kwa mfano, mkataba wa mchezaji unaisha mwaka huu na wewe usingepende
uingie tena kwenye makubaliano ya hela nyingine hapo unaweza kughushi, lakini
ni tabia ambayo haifai, ila ipo na sheria inakataza kufanya hivyo.
Haya yanayotokea ni bahati mbaya sana kwamba yanatokea
kwenye familia ya mpira ambayo inaheshimu utaratibu wake, angalia michezo
inapochezwa wakati wote kuna bendera ya ‘Fair Play’, mchezo wa kiungwana. Kama mkataba wa mchezaji
umekwisha kaeni naye tena, muingie mkataba mwingine, ukiisha na bado mna
mapenzi naye mnazungumza tena”.