Mshambuliaji mkongwe Mussa Hassan Mgosi, jana
alianza rasmi mazoezi na klabu yake mpya ya Simba kwa mkwara mzito ambapo
amewaahidi mashabiki wa timu hiyo kusubiri mambo mazuri kwa kuwaambia kuwa
amerejea Msimbazi kwa kazi na siyo maneno.
Mgosi aliyerejea SImba akitokea Mtibwa Sugar alikuwa injini na kuwaongoza wachezaji
chipukizi kwenye kila programu katika mazoezi hayo yanayoendelea kwenye Gym ya
Chang’ombe tangu Jumanne wiki hii yakisimamiwa na kocha msaidizi, Selemani
Matola.
Kuanza mazoezi katika siku ya kwanza tu
imeonyesha kuwa kweli Mgosi ni mmoja ya wachezaji wakomavu na wanaoyajua
majukumu yao.
Kwani idadi ya walioanza mazoezi ni wachache sana
ikionyesha wengi wataingia mazoezini baada ya siku mbili tatu au nne.
Lakini mkongwe huyo amekuwa kati ya wale walioanza mazoezi mapema jambo ambalo wengine wanapaswa kujifunza.