Timu
ya Taifa ya Brazil imechinjwa goli 1-0 dhidi ya Colombia katika mechi
ya pili ya kundi C ya michuano ya mataifa ya America kusini, Copa
America inayoendelea nchini Chile.
Goli
pekee la ushindi la Colombia kwenye mtanange huo uliochezwa uwanja wa
Santiago limefungwa dakika ya 36' kupitia kwa Jeison Murillo.
Dakika ya 90' Neymar wa Brazil na Carlos Bacca wa Colombia walioneshwa kadi nyekundu baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa.
Kadi
hiyo ni aibu kubwa kwa Neymar kwani haikuwa na ulazima ikizingatiwa
yeye ndiye nahodha wa Brazil na amebeba matumaini ya timu hiyo ambayo
bado ina machungu ya kupigwa 7-1 na Ujerumani katika mechi ya nusu
fainali ya kombe la dunia lililofanyika mwaka jana kwenye ardhi yao.
Tukio lilikuwa hivi: baada ya mwamuzi raia wa Chile, Enrique Osses kupuliza filimbi ya kumaliza mpira, Neymar alimpigia mpira kwa makusudi, Pablo Armero wa Colombia ambao ulimgonga mgongoni na ndipo vurumai ikaanza baina ya wachezaji wa timu zote mbili.
Wakati
fujo hizo za wachezaji zikiendelea, Carlos Bacca alimsukuma mgongoni
Neymar na ndipo mwamuzi akawaonesha kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Kwa mara nyingine tena, Radamel Falcao alionesha kiwango cha chini na alitolewa baadaye.
Mechi nyingine ya kundi C itapigwa usiku wa kuamkia kesho kati ya Peru na Venezuela.