Kocha
Mkuu wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, ni kama amewapoteza mastaa
wake wanaoitumikia Taifa Stars baada ya kutamka kuwa kwa sasa ‘anadili’
na wachezaji wanaohudhuria programu ya mazoezi tu.
Yanga
wanaendelea na programu hiyo katika Uwanja wa Karume jijini Dar
kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza mwezi ujao
jijini Dar, lakini kikosi hicho kilikuwa na wachezaji 10, wengine
wakiwa katika majukumu ya timu zao za taifa.
Wachezaji
muhimu wa Yanga, Simon Msuva, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Oscar Joshua,
Juma Abdul na Haruna Niyonzima, wapo katika timu zao za taifa, huku
wenzao wakiendelea na mazoezi.
Pluijm
alifafanua kwamba, kuwa na wachezaji wote katika programu ni jambo la
muhimu lakini kutokuwepo kwao hakuathiri chochote, labda kama kungekuwa
na mashindano makubwa ndani ya wiki mbili.
“Hapa
nia ni wachezaji wachache tu (10) wanaohudhuria programu yangu, wengi
wao wapo katika timu za taifa. Kwa kocha mwenye uzoefu kama mimi hili si
tatizo. Waache tu wafanye kazi, mimi ninajikita zaidi kwa hawa waliopo.
“Wachezaji
wakiwa nje ya programu wiki mbili kabla ya mashindano, hapo ndiyo
kunaweza kuwa na tatizo, lakini kwa vile bado tuna muda mrefu haina
shida, tena haina shida kabisa. Kila kitu kitakuwa vizuri,” alisisitiza
kocha huyo aliyewahi kuwa kipa wa timu ya taifa ya Uholanzi.
Katika
programu ya mazoezi ya jana asubuhi, Yanga ilikuwa na wachezaji kumi
pekee ambao ni Deus Kaseke, Edward Charles, Rajabu Zahir, Kelvin
Yondani, Benedict Tinoko, Hussein Javu, Pato Ngonyani, Geofrey
Mwashiuya, Lansana Kamara na Ally Mustafa ‘Barthez’