Goli
pekee la mshambuliaji Claudio Pizarro lilitosha kuwapa ushindi Peru
kwenye mchezo wa kundi C dhidi ya timu ya Venezuela kwenye michuano ya
Kombe la Amerika ya Kusini maarufu kama Copa America inayoendelea
kutimua vumbi nchini Chile.
Goli
hilo kutoka kwa straika wa Bayern Munich lililopachikwa kunako dakika
ya 72 lilikuwa na maana kubwa kwa Peru usiku wa kuamkia leo kwenye
michuano hiyo, kwasabu Peru wamepata ushindi wao wa kwanza hivyo kufufua
matumaini ya kusonga mbele kwenye kundi hilo lenye timu ngumu za
Brazil, Colombia pamoja Venezuela.
Peru
walistahili kushinda mchezo huo kufuatia Venezuela kucheza pungufu muda
mwingi wa mchezo kutokana na Fernando Amorebieta kulimwa kadi nyekundu
dakika ya 26 na kuacha Venezuela ikicheza pungufu muda wote wa mchezo.
Dakika
ya sita ya mchezo, Venezuela walifanya shambulizi kali ambapo mchezaji
Salomon Rondon alipata nafasi ya kufunga ikiwa ni mita nane toka langoni
lakini akaachia shuti ambalo liliishi mikononi mwa golipa wa Peru Pedro
Gallese ambaye aliunyaka mpira huo kiulaini.
Nafasi
peke kwa Peru kwenye kipindi cha kwanza ilikuwa ni dakika tano kabla ya
kwenda mapumziko lakini mshambuliaji Guerrero alipoteza nafasi hiyo kwa
kupiga shuti lilikwenda nje ya goli na kuikosesha Peru goli la kuongoza
kwa kushindwa kuitumia nafasi hiyo adimu.
Kipindi cha pili timu zote zilifunguka na kucheza soka safi huku Peru wakijitahidi kutengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli.
Wakati
mchezaji wa Venezuela Tomas Rincon akijitahidi kuokoa mpira uliopigwa
na Cueva ndipo mpira huo ukamkuta Pizzaro kwenye njia nae bila ajizi
akaukwambisha wavuni kwa shuti kali na kuipa timu yake ya Peru ushindi.
Ili
Venezuela waweze kusonga mbele, wanahitaji ushindi mbele ya Brazil ili
kujihakikishia wanafuzu kucheza hatua ya robo fainali. Peru wao
watakutana na Colombia ambao hawana pointi hata moja siku ya Jumapili
kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo.