RISHARD.
Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya miaka 15, Adolf Rishard, ameliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba kujiuzulu nafasi hiyo.

Adolf aliteuliwa na TFF miezi kadhaa iliyopita kuinoa timu hiyo ambayo imepangiwa mikakati maalumu ili iweze kukata tiketi ya kushiriki michuano ya vijana chini ya miaka 17 (U-17) itakayofanyika nchini Madagascar, mwaka 2017.
Adolf amesema amefikia hatua hiyo ya kuomba kujiuzulu baada ya kupata nafasi ya kwenda kuhudhuria kozi ya ukocha ambayo itamfanya aweze kutambulika kimataifa zaidi.
Alisema kutokana na kupata nafasi hiyo akaona aichangamkie haraka na kuiweka kando timu hiyo lakini akashindwa kutaja nchi ambayo anatarajia kwenda kuhudhuria kozi hiyo kwa kuwa anafuatilia nafasi katika nchi tatu tofauti, hivyo mpaka sasa hajajua ni ipi ataenda, akipata majibu ataweka wazi.
“Nina leseni A ya ukocha nikaona niende kuongeza elimu nipate ya ‘professional’, kozi hiyo ni ndefu, itanilazimu kukaa huko kwa miezi miwili. Siwezi kusema nitaenda nchi gani kwa kuwa zipo tatu lakini kozi itaanza baada ya mwezi wa Ramadhan,” alisema Adolf.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alithibitisha kupokea barua ya kocha huyo na kumtakia kila la kheri katika masomo yake na akaweka wazi kuwa, mchakato wa kumpata mrithi wake utafanyika mara moja.

AddThis

 
Top