Mshambuliaji wa Azam FC, Mcha Hamis, amewekewa bandeji ngumu P.O.P
kwenye mguu wake wa kushoto baada ya kupata majeruhi kwenye goti lake la mguu
wa kushoto, hivyo amepewa mwezi mmoja kuwa nje ya uwanja na atakosa mashindano
ya Kombe la Kagame.
Kwa mujibu wa Daktari wa Azam, Mbarouk Mlinga ni kuwa, Mcha atakaa
kwa kipindi cha mwezi mmoja nje ya uwanja.
“Alivunjika kidogo kwenye goti, ndiyo maana tukamwekea P.O.P ili awe
sawa. Atakaa na bandeji hiyo kwa muda wa wiki mbili na tangu alipowekewa hadi
leo, ameshamaliza wiki moja, hivyo Alhamisi ijayo atatolewa," alisema
Mbarouk.
Alisema wachezaji wengine ambao wana programu maalum ni beki wa kushoto, Waziri Salum aliyeumia unyayo, beki wa kati, Abdallah Kheri aliyechanika nyama ya paja na mshambuliaji Joseph Kimwaga aliyefanyiwa upasuaji Afrika Kusini lakini Farid Mussa aliyekuwa anasumbuliwa na nyama za paja amepona.