Mshambuliaji
wa Yanga anayeaminika kwa nguvu nyingi, Kpah Sherman, amefunguka kuwa
yupo tayari kuondoka klabuni hapo iwapo tu klabu yake itataka kumtoa kwa
mkopo.
Hivi
karibuni imeripotiwa kuwa, Yanga wapo kwenye mchakato wa kumtafutia
timu watakayompeleka kwa mkopo baada ya kutoridhishwa na kiwango chake
msimu uliopita.
Akizungumza
kutoka kwao Liberia jana, Sherman alisema kuwa katu hawezi kuwakatalia
kama wataamua hivyo, lakini ni mpaka arejee kwanza klabuni kwake na
kuangalia hali halisi.
“(Anacheka),
sina taarifa hizo lakini kama ni hivyo watataka niondoke, sawa tu maana
yatakuwa ni maamuzi yao. Lakini ni mpaka nikirudi Dar kuangalia hali
halisi ya mambo yenyewe.”
Wakati
huohuo, wakala wa nyota huyo wa zamani wa Cetinkaya ya Cyprus, Gibby
Kalule, alisema kuwa tayari kuna timu zimeonyesha nia kumhitaji lakini
kikwazo kikubwa ni mkataba wa miaka miwili alionao na Yanga.
“Kuna
timu zinamhitaji na mojawapo ni Bec Tero ya Thailand, ambayo ndiyo mpya
katika timu zilizovitiwa naye, lakini hakuna kilichofanyika kutokana na
mkataba wake na Yanga kuwa hai. Kama ikitokea ameruhisiwa, chaguo la
kwanza itakuwa ni hiyo,” alisema Gibby.
Wachezaji
wengine ambao wanatajwa kuwa kwenye mipango ya kupelekwa kwa mkopo ni
Hassan Dilunga na Charles Edward ambao wote wanatajwa kutakiwa na JKT
Ruvu.