Kikosi  cha Yanga, kesho Alhamisi, kinatarajia kuelekea mkoani Singida kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya wenyeji wao, Singida United, uliopangwa kupigwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Namfua uliopo Singida.
Msemaji wa Yanga, Dismas Ten amethibitisha juu ya safari hiyo kwa kusema maandalizi yote kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika na wanakwenda Singida wakiwa na matumaini ya pointi tatu.
“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri tangu kumalizika kwa mchezo dhidi ya Simba tumekuwa na mazoezi ya gym na juzi na jana tumefanya mazoezi ya uwanjani kwenye Uwanja wa Uhuru tukiamini yatatusaidia kupata ushindi huko tunapokwenda,” alisema Ten.
Msemaji huyo amesema ukiwatoa Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko wachezaji waliobaki wote wapofiti kwa ajili ya safari hiyo ya Singida.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina, amepania kushinda mchezo huo kutokana na kiwango bora walichokionyesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16, sawa na Simba iliyopo nafasi ya kwanza kutokana na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

AddThis

 
Top