Timu ya Simba haijawahi kushinda mechi mbili mfululizo kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, lakini safari hii kocha Joseph Omog ametamba kuvunja rekodi hiyo mbaya.
Kocha Omog ameandaa mpango mkakati maalumu ambao utakiwezesha kikosi chake kuibuka na pointi sita kwenye mechi mbili wanazokwenda kucheza Nyanda za Juu Kusini.
Akifafanua zaidi Omog alisema amepania kuhakikisha timu yake inavunja rekodi ya Yanga kwa kushinda mechi hizo mbili ingawa amekiri kuwa siyo jambo dogo.
Akinukuliwa, Omogo ambaye ni raia wa Cameroon alisema: “Msimu uliopita tulijitahidi kufanya hivyo lakini ilishindikana msimu huu tunaanza tena kucheza ugenini mechi zote mbili kwa ubora wa kikosi tulichokuwa nacho naamini tunaweza kuvunja rekodi ya Yanga.” 
Omog amesema anaziheshimu timu za Mbeya City na Tanzania Prisons, lakini msimu huu ataomba wawasamehe kwani wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima na hadhi ya Simba.
Simba inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam, siku yoyote kuanzia kesho kuelekea Mbeya ambapo Jumapili, itashuka kwenye Uwanja wa Sokoine kucheza na Mbeya City na baada ya mchezo huo itaendelea kubaki huko mpaka Jumamosi ijayo itakapo cheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja huohuo.

AddThis

 
Top