Hivi unadhani klabu ya Kagera Sugar inahangaika na dirisha hili dogo la usajili? La hasha! Licha ya kuonekana kuwa na matokeo ya kusuasua tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, klabu hio haina mpango wa kusajili kwenye dirisha hili.
Kocha Mkuu wa timu hio, Mecky Mexime amesema hana sababu ya kusajili mchezaji yeyote kwenye dirisha hili dogo kwani anaamini kikosi chake kina uwezo mkubwa wa kuendelea kujipapatua kwenye ligi hio na kupata matokeo.
Licha ya kukiri kuwa kikosi hicho hakina muenendo mzuri kwenye ligi, Mexime anaamini kuwa huo ni upepo mbaya tu unaokiandama kikosi hicho kwa hivi sasa lakini upepo huo utakapotulia matokeo mazuri yatapatikana.
“Hapana, wachezaji wangu nilio nao nitaendelea kubaki nao, ni matokeo tu ya kimchezo, ni upepo tu mbaya umetupitia lakini ninaamini nina wachezaji wazuri na sina sababu ya kuongeza wengine,” alisema Mexime.
Kagera Sugar ipo kwenye nafasi ya 10 baada ya kushuka dimbani kwenye michezo 10 ikishinda michezo miwili, kwenda sare kwenye michezo minne na kupoteza michezo minne katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Licha ya kutohitaji kusajili, Mexime anakabiliwa na changamoto kwenye eneo lake la ushambuliaji kwani halina uhakika wa kufunga mabao mengi huku wafungaji tegemezi kwenye kikosi hicho wakiwa ni Venance Ludovick na Edward Christopher ‘Edo’.

AddThis

 
Top