Mugabe, 93, amekuwa kiongozi wa Zimbabwe tangu mwaka wa 1980.
Alikuwa Waziri Mkuu hadi 1987 alipochukua usukani kama rais wa nchi hiyo. Utawala wake wa miaka 37 umeshutumiwa kwa ukandamizaji wa upinzani, ukiukaji wa sheria za uchaguzi, na kusababisha uchumi wa nchi kuanguka.
Yafuatayo ni mambo tisa ambayo huenda hukuwa unayajua kumhusu kiongozi huyu.
1) Hapendi kushindwa
Alipokuwa kijana, Mugabe alikuwa mmakinifu na mzuri kabisa katika mchezo wa tenisi, kulingana na aliyekuwa mwalimu katika shule ya Wakatoliki alikosomea Mugabe. Ila, aliposhindwa katika mchezo huo, aliitupa raketi yake chini kwa hasira.
Mugabe amekiri kuwa hakuwa mzuri katika mchezo wa kandanda alipokuwa mdogo, ila kwa sasa, anapenda kuutazama mchezo huo.
Yeye ni shabiki wa klabu za Chelsea na Barcelona.
2) 'Kufufuka'
Kuhusu afya yake, Mugabe alipohojiwa wakati mmoja alisema," Nimekufa mara nyingi-hapo ndipo nimemshinda Yesu Kristo. Yesu alikufa mara moja, na akafufuka mara moja," alisema alipotimiza miaka 88.
Ingawa alilelewa katika familia ya Kikatoliki, alisema alipohojiwa na kituo cha habari cha Afrika Kusini, SABC, miaka michache iliyopita, kuwa yeye si Mkristo anayetumikia dini kwa sana.
3) Shabiki mkubwa sana wa kriketi
Kwa muda mrefu amedhihirisha hadharani mapenzi ya mchezo wa kriketi. Ni mlezi wa jumuiya ya mchezo wa kriketi wa Zimbabwe na nyumba yake ipo karibu na uga wa michezo wa Harare.
"Kriketi yafanya watu wawe wangwana, na pia inawafanya watu kuwa wema," Bw Mugabe alisema miaka kadhaa baada ya Zimbabwe kujinyakulia uhuru. "Nataka kila mtu acheze kriketi Zimbabwe; nataka nchi ya Zimbabwe iwe nchi ya wangwana."
4) Mazoezi na vyakula vya kienyeji
Mugabe anapenda kufanya mazoezi. "Mimi hujihisi mgonjwa wakati sijafanya mazoezi ya viungo vya mwili," Bw Mugabe alisema miaka sita iliyopita. Huwa anaamka kati ya saa kumi na kumi na moja alfajiri. Siri nyingine ya maisha yake marefu ni kuwa anapenda sana 'sadza' - chakula cha kienyeji kinacholiwa sana Zimbabwe, na ambacho kina virutubisho vingi muhimu. Vilevile havuti sigara, ingawa hunywa pombe kidogo anapokula chakula cha jioni.
5) Alipata mtoto akiwa miaka 73
Ana watoto watatu na mke wake wa pili, Grace Marufu, aliyekuwa karani wake. Mtoto wao wa tatu alizaliwa 1997, mwaka mmoja baada ya wao kufunga ndoa.
Mwanawe wa kwanza, Nhamodzenyika, alikufa kutokana na Malaria akiwa na umri wa miaka mitatu Mugabe alipokuwa mfungwa wa kisiasa wa serikali ya enzi hiyo ya Rhodesia.
6) Anampenda Cliff Richard kumliko Bob Marley
Mwanasiasa wa Zimbabwe ambaye kwa sasa ni hayati, Edgar Tekere, alimwambia mwandishi wa BBC, Brian Hungwe, kuwa alipokuwa akitayarisha kadhia ya kusherehekea uhuru wa Zimbabwe 1980, Mugabe hakumtaka mwimbaji Bob Marley aalikwe kutumbuiza watu, ila alimtaka muimbaji maarufu wa Uingereza, Cliff Richard. Pia anampenda Mwimbaji, Jim Reeves.
7) Mvaaji wa nguo maridadi
Anapenda sana suti zinazoutosha mwili wake sawasawa na tai zinazofanana na kitambaa. Huwavutia sana wanamitindo nchini Zimbabwe kwa mavazi yake.
8) Anamtazama Kwame Nkrumah kama kielelezo kwake
Bw Mugabe alipata azma ya siasa akiwa Ghana alipokuwa mwalimu; mahali alipokutana na mke wake wa kwanza, Sally Hayfron.
Aliporudi Zimbabwe, aliwaambia wananchi jinsi Ghana ilivyojinyakulia uhuru na jinsi uhuru ni kitu kizuri.
Katika mahojiano mwaka 2003, Mugabe alisema: "Niliwaambia pia kuhusu Kwame Nkrumah jinsi alivyojitolea na kuiongoza Ghana kupata uhuru; Kwame aliwaambia wananchi wa Ghana kuwa Ghana haingekuwa nchi huru bila ya jitihada na kujitolea kwa kila mtu.
9) Ni mtu mwenye shahada nyingi
Kwa jumla, Mugabe ana shahada saba. Digrii yake ya kwanza ni kutoka chuo kikuu cha Fort Hare, Afrika Kusini. Alisomea shahada zake nyingine kupitia mtandao akiwa gerezani.
Shahada hizo ni za: elimu, sayansi, sheria na usimamizi.