Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe amesema kuwa kukaa nje muda mrefu Kuna mfanya awe na hamu ya kurudi uwanjani kwa kasi.
Mshambuliaji huyo ambaye alitokea Klabu ya Vitalo ya Burundi kabla ya kujiunga na Simba kisha Yanga, ameshawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom akiwa na timu mbili tofauti.
Tambwe amesema amekuwa akiifuatilia kwa karibu timu yake na kupatwa na midadi jambo ambalo linamfanya awe na hamu kubwa ya kurudi dimbani ili kusaidiana na wachezaji wenzake katika kupigania mafanikio ya mabingwa hao.
"Naumia sana kuona nipo nje na wenzangu wanaendelea kupigika, ninachokwambia kwa sasa ni kurudi kazini mapema iwezekanavyo ili kuungana na wenzangu tuweze kuipigania timu yetu kwa Mara ya nne mfululizo," alisema Tambwe.
Mshambuliaji huyo raia wa Burundi amesema kazi kubwa tayari ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi zinazofuata lakini kitu cha msingi ambacho kipo mbele yake ni kuangazia namna ya kuongeza nguvu wakati huu ambapo Ligi imekuwa na ushindani mkubwa.
Amesema kwa mtazamo wake Yanga bado ni timu imara nchini na ina uwezo wa kufanya vizuri hata kwenye michuano ya kimataifa hivyo kitu cha msingi ni maandalizi mazuri ili waweze kutimiza malengo ya timu.
Tabwe hajaichezea Yanga tangu kuanza kwa msimu huu na tatizo kubwa linalomkabili ni maumivu ya goti ambayo aliyapata kisiwani Pemba wakati wakijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

AddThis

 
Top