Baada ya taarifa kusambaa kuwa mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma alisafiri bila kuaga, uongozi wa klabu yake umesema kuwa unamsubiri mchezaji huyo ili ajieleze juu ya safari yake ya kwenda kwao, Zimbabwe.
Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten amenukuliwa akisema kuwa kuondoka kwa Ngoma ni suala la ukweli lakini uongozi utatoa tamko mara baada ya mchezaji huyo kurejea na wao kumpa nafasi ya kumsikiliza kabla ya kuchukua hatua nyingine.
“Ngoma alikuwa Zimbabwe wakati wowote kuanzia sasa anaweza kufika, alikuwa na matatizo ya kifamilia, taarifa za kuondoka kwake ndiyo zina mkanganyiko. Siku zote mchezaji anapotoka anaaga kwa mwalimu na taarifa zake zinafikishwa kwenye uongozi, hakukuwa na taarifa zake rasmi ofisini, tunasubiri afike ili hatua nyingine ziweze kuchukuliwa,” alisema Dismas.
Ofisa habari huyo aliendelea kusema kuwa hawezi kutamka kitu zaidi ya hapo kwa kuwa Ngoma ni binadamu kama wengine, kwa hiyo wanapaswa kumsikiliza na kujua nini kilikuwa kina mkabili ili hatua nyingine baada ya hapo ziweze kufuata.
Ngoma amecheza mechi nne za kwanza za Yanga msimu huu kati ya tisa, alikosekana kwenye mechi nyingine tano (5) kutokana na kuuguza majeraha aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo alishindwa kuendelea na mchezo huo na kulazimika kupumzishwa. Amefunga mabao mawili katika mechi nne alizocheza msimu huu.

AddThis

 
Top