Uongozi wa timu ya Azam FC umepinga kitendo cha kamati ya utendaji ya TFF kutoza kiasi cha dola 2,000 za kimarekani kama ada ya maendeleo ya soka la vijana kwa kila mchezaji wa kigeni atakayesajiliwa.
Mtendaji mkuu wa Azam FC Saad Kawemba amesema, ada hiyo kwa wachezaji wa kigeni ambao watasajiliwa kucheza kwenye ligi kuu Tanzania bara ni sawa na kuvikomoa vilabu kwasababu vyenyewe ndio vilitaka ongezeko la wachezaji kutoka watano.
“Kwanza kabisa tunamasikitiko kwasababu jambo kama hili ambalo linatuhusu moja kwa moja hatukuitwa, hatuzungumzi halafu linakuwa ni tamko, moja kwa moja maana yake ndo inakuwa sheria kwakweli inakuwa haileti tija sana”, amesema Kawemba.
 “Halafu tukizungumza hawa wachezaji wageni ni wangapi ambapo unataka upate dola 2,000 kwa kila mmoja kwa mwaka na shughuli za mpira wa vijana zinataka pesa kiasi gani, yani kama tungekaa chini kwa nafasi, tungeweza kuelekeza vyanzo vingine bora zaidi kuliko kwenda huko”, ameongeza.
“Ni masikitiko makubwa sana kuona inakuwa ni kanuni na sheria kwamba ni lazima ifanyike hivyo, vilabu vinaingia gharama kubwa kuwaleta hawa wachezaji vinawalipa mishahara, kuwatafutia sehemu za kuishi halafu bado tunalipia hata vibali vyao vya kufanya kazi hapa nchini ambalo ni jukumu la kierikali na sasa TFF na wao wanataka waweke kodi nyingine juu ya kodi za serikali”, amefafanua.
“Kidogo inaleta ukakasi kwa maana ya utendaji wake lakini bado tunasema ni mapema mno, tunaamini nafasi bado ipo ya kujadiliana, tunaweza kujadiliana na kufikia muafaka. Kuna vikao na sisi kama vilabu tuna nafasi yetu ya kuzungumza, tunaweza tukapeleka kwenye vikao halali litajadiliwa na naamini kabisa hekima au busara itapatikana na mwelekeo mzuri utapatikana siyo kutamka tu na mwisho inakuwa ni kanuni”, amesema.
“Kwasababu kila tukicheza mechi tunalipa asilimia sita kwa ajili ya kuendeleza soka la vijana, na anaefanya soka la vijana ni nani, ni TFF au ni vilabu? Sasa vilabu bado tunaingia gharama za hawa vijana kwasababu sisi ndio tunakuwa na ‘camp’ za hawa vijana, ‘academy’ zote zipo kwetu TFF hawana jukumu la kuwa na academy sio jukumu lao kabisa. Soka la vijana ni jukumu la vilabu, sasa vilabu bado vinatoa pesa kwenye soka la vijana kwenda shirikisho”, Kawemba alimaliza.
Vilabu vilitoa pendekezo kwa TFF kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni ili iwe changamoto kwa wachezaji wa ndani kufanya vizuri lakini pia vilabu vipate uwezo wa kupambana na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa. Siku chache zilizopita, TFF ilitangaza kuridhia ombi hilo na kuongeza idadi ya wachezaji hadi kufikia saba toka watano ambao wanaweza kusajiliwa kwenye klabu moja na wote kuruhusiwa kucheza kwa wakati mmoja kwenye mchezo mmoja.

AddThis

 
Top