Bodi ya timu ya Mtibwa Sugar imeshindwa kukutana na kufanya kikao chake wiki hii kutokana na viongozi wa bodi hiyo kutokuwepo kwa pamoja, lakini klabu hiyo ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro imesema iko mbioni kufanya kikao hicho mapema iwezekanavyo ili kujadili masuala mbalimbali yahusuyo klabu hiyo ya wakata miwa.
Afisa habari wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema, kikao cha bodi ya timu hakikufanyika kama ilivyopangwa kutokana na kutokuwepo kwa wajumbe wengi wa bodi hiyo ambao wengi wao walikuwa nje ya nchi. Lakini ameahidi kuwa, kikao hicho kitafanyika muda wowote kuanzia sasa ili kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo.
“Kikao chetu cha bodi ya timu ya Mtibwa Sugar ambacho kilikuwa kifanyike juma hili ambacho kingejadili masuala mbalimbali ya ushiriki wa klabu ya Mtibwa katika ligi kuu kwa msimu wa 2015-2016 kimeshindikana, lakini tuko mbioni kukifanya kikao hicho”, amesema Kifaru.
“Tulikuwa tukiwasubiri wenzetu ambao wengi wao walikuwa nje ya nchi lakini tunategemea wakati wowote kuwa na kikao hicho cha bodi. Wakati huo tukisubiri kikao hicho cha bodi, uongozi wa Mtimbwa Sukari unaendelea na mazungumzo ya kuwashawishi wachezaji wetu tuliokuwa nao kwenye msimu wa 2014-2015 ili tuendelee kuwa nao”, amefafanua.

AddThis

 
Top