Kikosi
cha African Sports ‘wanakimanumanu’ kimethibitisha kumsajili aliyekuwa kocha
msaidizi wa timu ya Kagera Sugar Mrage Kabange kwa ajili ya kukinoa kikosi chao
kitakachoshiriki ligi kuu Tanzania bara kwa msimu ujao
Katibu
mkuu wa African Sports Khatibu Enzi amethibitisha kumnasa kocha huyo akisema
kuwa, kila kitu kinakwenda sawa na tayari wamempa mkataba kocha huyo ili ausome
na kama akiridhia watasaini mkata wa mwaka mmoja kwa ajili ya kukinoa kikosi
hicho.
“Mazungumzo
na Mrage Kabange yameshamalizika, nimemkabidhi mkataba ausome na yeye auhakiki
baada ya hapo kilichobaki ni kufunga mkataba. Tumeongea nae na tumekubaliana atasaini mkataba wa mwaka
mmoja”, amesema Enzi.
“Kilichotuvutia kwa kabange tuliona timu ya Kagera Sugar
ipo kwenye ligi kwa muda mrefu, haiyumbi, inacheza mpira mzuri ambao ni mpira
bora, katika hali hiyo tukapata mapendekezo ya kumuita Kabange aje aisaidie
timu ya African Sports”, ameongeza.
“Lengo kuu ilikuwa ni kumpata Bakari Shime lakini
kwasababu tulimkosa kamati ikaamua kutafuta kocha mwingine ikampata Kabange na
kumleta Tanga, nadhani atatusaidia”, amesema.
“Kwasasahivi timu inaendelea vizuri imeshaanza mazoei
takribani wiki mbili na kwasababu mwalimu tayari yupo, basi tutatangaza usajili
rasmi”.
Kwa upande wake Kabange yeye amesema, kilakitu kinakwenda
sawa na baada ya muda mfupi mambo yote yatakuwa sawa na atakuwa kocha mkuu wa
kikosi cha African Sports.
“Tupo kwenye mazungumzo na viongozi wangu hapa lakini kilakitu
kinakwenda sawa na naamini mambo yatakwenda vizuri, baada ya siku chache kila
kitu kitakuwa sawa na nitakuwa kocha mkuu hapa”.
Kabange amekuwa kocha msaidizi kwenye kikosi cha Kagera Sugar kwa muda wa miaka nane lakini sasa anapewa majukumu ya kuwa kocha mkuu kukiongoza kikosi cha wanakimanumanu kwenye ligi kuu msimu ujao na atakutana na aliyekuwa bosi wake Jackson Mayanja wakati wakikinoa kikosi cha Kagera Sugar ambaye kwa sasa yupo Coastal Union. Na watakutana kwenye Tanga ‘Derby’ kati ya Coastal Union dhidi ya African Sports.