NIWAKUMBUSHE kwamba, tunapokwenda sasa ni pabaya, maana tunaanza kuondoka katika afadhali na kutumbukia kunakoonekana ni mwisho kabisa wa shimo.

Najua utakuwa umesikia taarifa za mashabiki kulishambulia gari la wachezaji wa Taifa Stars wakati wakiwa barabarani wakienda mazoezini.
Walifanya hivyo mara ya kwanza hadi wakapasua kioo, jambo ambalo kwangu nililiona ni la kusikitisha pale unaposikia wananchi wanaamua kuwashambulia wanajeshi wao, tena wakiwa katika maandalizi ya kwenda kupambana na adui ambaye hajulikani yuko katika ubora upi.
Nilijiliuza, wanaolishambulia basi hilo ni wananchi wa aina gani ambao wanaweza kuonyesha mapenzi yao kwa kuwaumiza wadogo au kaka zao ambao ndiyo wanaokwenda kupambana kwa ajili ya taifa lao?
Jibu haliwezi kupatikana kirahisi, wakati mwingine unafikiria aliyefanya hivyo anaweza kuwa ni Mtanzania wa kuchovya, huenda anatokea nchi jirani!
Kama ana hasira, basi angeweza kukaa kimya. Ikiwezekana akasusa na kuacha kuishangilia timu kuliko kuishambulia. Mimi pia nachukizwa na mwenendo wa Stars, lakini ndiyo timu ya nchi yangu. Kamwe kama mkono wako ukinyewa, hauwezi kuukata. Inaendelea kubaki ni timu yangu ya taifa.
Juzi likatokea tukio jingine baada ya shabiki mwingine kulishambulia basi la Stars likiwa katika makutano ya barabara za Uhuru na ile ya kwenda gerezani. Basi likasimamishwa, wachezaji na baadhi ya watu wa benchi la ufundi wakateremka na kuanza kumkimbiza mhusika, wakamkamata na kumtandika.
Kweli kupigwa kila wakati inaudhi, lakini najiuliza sasa wachezaji nao wameanza kupiga mashabiki? Unaweza vipi kuwatofautisha na ule ujinga wa shabiki aliyeshambulia basi la Stars?

Shabiki mpuuzi kashambulia na wachezaji nao wamefanya upuuzi huohuo wa kushuka na kumshambulia shabiki! Sasa nani anasalimika katika upuuzi huu?
Tumepiga hatua mbovu kabisa, kwamba sasa imekuwa ni vita kati ya mashabiki wanaofanya upuuzi dhidi ya wachezaji wetu wa timu ya taifa wanaofanya upuuzi zaidi, tena mbele ya viongozi wao walioshindwa kuwadhibiti. Nidhamu ni mbovu?
Huenda mashabiki walikuwa na ujumbe wa kufikisha kwa wachezaji kwamba pamoja na ubovu wa kocha Mholanzi, Mart Nooij, nao pia hawajitumi au hawana msaada na timu na wanapaswa kubadilika.
Lakini walichukua njia ambayo si sahihi kwa kulishambulia basi, jambo ambalo si sahihi kisheria, si vema kiungwana na si tabia za Kitanzania. Kila mtu ana hasira, wakati mwingine vizuri kuzizuia.
Wachezaji kweli nao ni binadamu, wanaweza kukerwa na tabia ya kushambuliwa, huenda wanaona hawana kosa na si haki wao kushambuliwa. Sahihi kabisa, lakini tunabaki palepale kwamba bado wangeweza kumkamata mtu huyo, halafu wakamkabidhi kwenye vyombo vya dola, si walivyofanya wao, tena wakionekana ni watu muhimu katika kupigania na kulinda heshima ya nchi yetu.
Umeona tulipo sasa! Wachezaji wa timu ya taifa na mashabiki wa timu ya taifa kuwindana mitaani, tena hata kabla ya mechi na kuchapana.
Jambo baya kabisa katika picha ya soka ya Tanzania na hii inaonekana kiasi gani sisi ni wajinga na tusiojitambua. Hatujui tuendako, si watu tunaoweza kuheshimiana au kutumia njia sahihi za kufikishiana ujumbe au kukatazana jambo.
Kizazi hiki kinaonekana kuwa na wazembe wengi ambao wazi hawawezi kukisaidia kusonga mbele. Wachezaji wasio tayari kupambana vilivyo kwa taifa lao, huenda kwa sababu posho imechelewa au kwa kuwa hawajiamini tu.
Mashabiki walio tayari kuishambulia timu yao ya taifa ikiwa katika maandalizi ya mechi muhimu dhidi ya Uganda kuwania kucheza Chan. Inawezekana ndiyo ujinga tuliozaliwa nao, lakini mwanadamu bora ni yule anayebadilika.
Kweli Stars imepoteza, sasa mechi inayokuja kinachotakiwa ni kuwapa moyo, si kuwashambulia kwa mawe. Tutumie njia sahihi kuwafikishia ujumbe.

Wachezaji nao, oneni aibu basi. Kila siku nyie tu, mambo ya kubahatisha tu! Kama mnaona Mholanzi wenu uwezo wake ni mdogo, mshauri wa ufundi wa Rais wa TFF naye ni mchanga na hana msaada wowote, basi tumieni uwezo wenu binafsi na muisaidie timu. Kweli tunaumia na watu wanachoka. Aaah!

AddThis

 
Top