Kikosi cha Simba, jana Jumanne kilianza mazoezi yake ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni siku moja tu tangu wamtangaze kocha wao mpya, Muingereza, Dylan Kerr anayetarajiwa kuwasili nchini wikiendi hii.
Simba
ambayo msimu uliopita wa ligi ilimaliza nafasi ya tatu, imeanza mazoezi
ya gym chini ya kocha wao msaidizi, Seleman Matola, huku ikiwa na
wachezaji wachache kutokana na wengine kuwa mbali na Dar ambapo mazoezi
hayo yatadumu mpaka hapo atakapowasili kocha mkuu.
Matola
amesema kuwa jana Jumanne kikosi hicho kilianza mazoezi yake ya
kujiwinda kwa msimu wa ligi kuu rasmi kwa kuanzia gym ambapo watadumu
katika mazoezi hayo mpaka watakapoingia kambini rasmi.
“Ndiyo
tumeanza mazoezi kidogokidogo ya gym ambapo tutakuwa tukifanya kila
siku asubuhi kwenye gym iliyopo Chang’ombe tukisubiri kuingia kambini
kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
“Ingawa tumeanza mazoezi lakini idadi ya wachezaji ni ndogo kutokana na wachezaji wengi kuwa mbali na hapa Dar, lakini mpaka wiki ijayo watakuwa wamesharejea kwani kambi rasmi ndiyo itakuwa inaanza,” alisema Matola