KASEKE NA MWASHUYA WAKIWA MAZOEZINI.
Viungo washambuliaji wapya wa Yanga, Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya taratibu wameanza kuingia kwenye kikosi cha kwanza Mholanzi, Hans Pluijm, atakachokitumia kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wachezaji hao wote wanacheza viungo washambuliaji wanaotokea pembeni kwa upande wa Kaseke yeye anacheza namba 7 inayochezwa na Simon huku Mwishiuya akicheza 11 ambayo kwenye msimu uliopita ilikuwa ikichezwa na Andrey Coutinho.

Kaseke amejiunga Yanga hivi karibuni akisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Mbeya City huku Geofrey Mwashiuya aliyetokea Kimondo FC  iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Katika mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Pluijm alionekana akiwapa mbinu mbalimbali za ndani ya uwanja viungo hao.

Kocha huyo, aliwapa mbinu za jinsi ya kupiga krosi kwa washambuliaji kabla ya kufunga mabao wakati timu inashambulia goli la timu pinzani.

Wakiendelea na mazoezi hayo, kocha huyo alisikika akiwataka viungo hao kuinua macho na kuwaangalia washambuliaji wao kabla ya kupiga krosi hizo ili mpira umfikie mchezaji mwenzake.

Viungo hao, pia wakati mwingine walitakiwa kufunga wenyewe mabao pale wanapopata nafasi ya kupiga mashuti ndani au nje ya 18 ya uwanja.

Akizungumzia mbinu hizo, kocha huyo alisema kuwa :“Mazoezi ya stamina, nguvu na pumzi tayari nimemaliza na nilichobakisha hivi sasa ni mazoezi ya mbinu ya jinsi ya kufunga na kuzuia mabao golini kwetu.

“Mazoezi hayo ya mbinu nitaendelea nayo kwa kipindi kirefu, kama unavyoona tumesajili wachezaji wapya ambao bado hawajaujua mfumo ninaoutumia, hivyo natumia muda huu kuwapa mbinu nitakazozitumia,”alisema Pluijm.

Aidha katika hatua nyingine, Pluijm alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa kikosi chake kwenye msimu ujao wa ligi kuu kuwepo na mabadiliko baada ya kusajili wachezaji wapya.
Mbali na hawa wachezaji wengine ambao walikuwa na kina Kaseke ni Kpah Sherman, Salum Telela, Malimi Busungu na  Juma Abdul.

AddThis

 
Top