Rasmi sasa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm,
ametangaza rasmi kwamba, hana mpango wa kumsajili kiungo aliyekuwa akifanya
majaribio kikosini hapo, Msierra Leone, Lansana Kamara, ila akatamka kauli ya
kishujaa kuwa ndani ya wiki hii atakamilisha usajili wa wachezaji wawili wa
kimataifa.
Kamara aliyekuwa akijifua Yanga kwa wiki tatu mfululizo,
ametemwa kikosini hapo baada ya majaribio ya mechi ya kwanza ya kirafiki
waliyocheza na Friends Rangers ya Magomeni kwenye Uwanja wa Karume, juzi
Jumatano.
Mchezaji huyo alipewa taarifa hiyo rasmi na kocha
huyo jana ambapo alimuweka wazi kuwa katika mechi hiyo ya kwanza ya mazoezini
hakuonyesha kitu, hivyo anapaswa kuchagua mawili, aidha kuendelea kujifua na
Yanga bila matumaini yoyote ya kuichezea timu hiyo msimu ujao au aangalie
maisha sehemu nyingine.
Imeelezwa kuwa kauli hiyo ilimchefua mchezaji
huyo na kuamua kukacha mazoezi ya Yanga yaliyoendelea jana Karume kwa ajili ya
maandalizi ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda, utakaopigwa
kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
“Kamara nimemwambia kwamba kwa kiwango
alichonionyesha mazoezini na kwenye mechi ya juzi ni cha kawaida sana kwa
mchezaji profesheno kama yeye, halafu pia kiwango chake hakikuweza kuzidi
viungo nilionao hapa. Kwa staili hiyo sitaweza kumsajili mchezaji wa kiwango
kama chake.
“Kwa hiyo nikamwambia anaweza kuja kuendelea
kufanya mazoezi na sisi kama kawaida lakini sitamchukua, sasa sijajua imekuwaje
kama ameacha kufanya mazoezi au ni vipi kwa sababu leo (jana) sijamuona hapa,
hata hivyo hainisumbui kitu kwa sababu nilishamweleza ukweli wake,” alisema
Pluijm.
Alipoulizwa kama timu pinzani za ligi kuu
zikimnasa Kamara itakuwaje, alisema: “Wamnase tu (anacheka kuonyesha hajali),
kwa mpira alionao sidhani kama ataweza kusumbua safu ya viungo wangu, aende tu
hata Simba, Azam au timu nyingine yoyote hakuna tatizo.”
Katika mazungumzo hayo, Pluijm hakuishia hapo tu,
bali aliongeza kuwa kuanzia leo Ijumaa, ndani ya siku tatu lazima asajili
wachezaji wawili wenye viwango vya juu kutoka nje.
“Kuna wachezaji wawili wanakuja, nikuhakikishie
tu kwamba wiki hii haiishi yaani haifiki Jumapili, kuna wachezaji profesheno
tunamalizana nao na wana viwango vizuri tu, sikutajii nchi gani wala wanacheza
nafasi gani ila utawaona tu. Nakuhakikishia tena kwamba kabla ya wiki hii
kuisha,” alimalizia Pluijm.
Wiki iliyopita gazeti hili liliweka wazi kuwa Kamara hana nafasi ya kuichezea Yanga kutokana na kuonyesha uwezo wa kawaida licha ya baadhi ya wadau walio karibu na timu hiyo kuonekana kumpigia debe, hivyo neno limetimia.